Na Greyson Mgoi
Watende Ramadhani Botea, Mkazi wa Kijiji cha Makulunge ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Shule ya Msingi Migiro iliyopo Kata ya Makulunge, Wilayani Bagamoyo, Pwani anasema mafunzo ya Elimu ya Stadi za Maisha na Maadili aliyoyapata kutoka Shirika la Uwezo Tanzania yamembadilisha kwa kiasi kikubwa na kumsaidia kuweza kuwalea na kuwajenga watoto wake kukua vizuri huku wakiwa na mahiri na stadi muhimu katika maisha yao.
Watende anasema kabla hajapata mafunzo hayo alikuwa hajua hata nini maana ya Stadi za Maisha, ambapo mara baada ya kupata mafunzo hayo kutoka kwenye mradi wa Stadi za Maisha na Maadili Africa Mashariki (Action for Life Skills and Values in East Africa-ALiVE) ameweze kuelewa kuwa stadi za maisha ni mahiri wezeshi zimsaidiazo mtu kuweza kukabiliana na mazingira mbalimbali ya kila siku.
Anasema mafunzo ya Stadi za Maisha yamemsadia katika kukuza uelewa wake juu ya mahiri mbalimbali mfano, kuwasiliana, kushirikiana na watu wengine vema katika jamii na pia kukuza uwezo wake wa namna ya kutatua matatizo pale yanapo mkabili.
Akitolea mfano juu ya stadi ya Utatuzi wa Matatizo, anasema ameelewa kuwa ukipatwa na tatizo ni muhimu kufuata hatua muhimu za kutatua tatizo ili uwezo kulitatua kwa usahihi, ambapo anasema hatua muhimu ya kwanza ni kuweza kulitambua tatizo lenyewe kuwa ni tatizo ndipo unaanza kufikiria njia mbalimbali za namna ya kulitatua.
Anasema, baada ya kujifunza na kufahamu vema mahiri hizo muhimu ikiwemo hii ya utatuzi wa mtatizo, kwa sasa ameweza kuwasadia watoto wake kukuza ujuzi wa kutatua matatizo, na amewajengea tabia ya ujasiri na kujiamini. Anasisitiza kuwa stadi hii ni muhimu sana inamuwezesha mtoto kutatua changamoto mbalimbali zinazomkabili katika maisha yake.
“Pia nilipata nafasi ya kuweza kuwashirikisha wenzangu wengine kuhusu mafunzo niliyopata ya stadi za maisha na maadili, niliwashirikisha tukiwa kwenye mikutano ya kijiji na kwa kweli wazazi wengi walivutiwa nae limu hii” Anasema Watende.
Watende anatoa wito kwa wazazi wengine kuwasaidia watoto wao kukuza stadi hizi muhimu kwa kuwa stadi za maisha zina faida na zinasaidia sana katika malezi bora ya watoto.
Akifafanua kuhusu mafunzo waliyopata kuhusu Stadi za Maisha na Maadili hasa stadi ya utatuzi wa Matatizo alisema walifundishwa kama Mzazi/Mlezi unapaswa kufanya mambo yafuatayo ili kumsaidia mtoto kukuza stadi ya Utatuzi wa Matatizo, ambapo mambo hayo ni;- Kuwaruhusu watoto kujitatulia matatizo yao wenyewe, mafano mtoto akija na tatizo badala ya kumsaidia, muulize anawezaje kutatua tatizo hilo?, Pia kuwahimiza watoto kutafuta taarifa zaidi kuhusu tatizo husika, na kuwahimiza watoto kutumia taarifa walizonazo ili kuweza kupendekeza njia mbalimbali za kutatua tatizo husika, kuwahimiza watoto kuangalia mbinu gani inaweza kutatua tatizo husika kwa ufanisi, na kuwahimiza watoto kujaribu mbinu hiyo na kama haifanyi kazi kujiuliza kwanini na kuangalia mbinu gani mbadala inaweza kutatua tatizo hilo.
Akitoa wito kwa jamii na serikali watende anaomba elimu hii iweze kufikishwa kwa kila mtu, kwa wote wazazi na watoto kwa kuwa imekuwa masaada mzuri sana kwake na wazazi wengine vinara zaidi ya 40 ambao walipatiwa mafunzo hayo wilayani Bagamoyo na badae wakaenda kuwashirikisha wazazi wengine.
“Wito wangu kwa serikali ma jamii kwa ujumla, elimu ya stadi za maisha na maadili ni muhimu kwa kila mtu, nashauri kila mtu ajifunze na ikiwezekana watoto wote wafundishwe elimu hii wakiwa shuleni na nyumbani” Alisistiza Watende.
Kwa mujibu wa ripoti ya utekelezaji (2025) wa kampeni ya wiki kumi ya Utatuzi wa Matatizo iliyotekelezwa chini ya Mradi wa Stadi za Maisha, na Shirika la Uwezo Tanzaia kwa Kushirikiana na mashirika wadau wake OCODE (Bagamoyo), Milele Zanzibar(Zanzibar) na SAZANI Trust (Zanzibar), lengo kuu la kampeni hiyo ilikuwa ni kuimarisha ushiriki wa wazazi na jamii katika kukuza utatuzi wa matatizo na ujuzi wa maisha miongoni mwa watoto na vijana kupitia kampeni ya kitaifa ya wiki kumi, pia kukuza utamaduni wa uchunguzi, ubunifu, ustahimilivu, na ujifunzaji endelevu.
Sambamba na lengo kuu, miongoni mwa malengo mahususi ya kampeni hiyo yalikuwa;- Kuwahimiza wazazi na jamii kukuza udadisi wa watoto na ujuzi wa kuuliza maswali ili kukuza mawazo makini, Kujumuisha shughuli za vitendo na zinazofaa kwa umri wa shuleni na nyumbani ili kuwasaidia watoto kutumia ujuzi wa kutatua matatizo katika muktadha halisi, na pia kukuza mawazo ya ubunifu kupitia sanaa, michezo, na uvumbuzi ili kujenga kujiamini kwa watoto, na uwezo wa kutoa suluhisho mbadala.

Washiriki( Wazazi Vinara) wakijifunza juu ya stadi ya utatuzi wa matatizo_ mafunzo hayo yalifanywa na maofisa wa Mradi wa stadi za maisha ya maadili huko Zanzibar .
Ripoti hiyo inabainisha kuwa, Idadi ya wadau waliofikiwa na kunufaika na kampeni hii, huko Zanzibar, kampeni hiyo iliwafikia moja kwa moja watu 3,144 ambao kati yao 1,063 walikuwa wanaume na 2,081 wanawake, huku ikihusisha kikamilifu wazazi (949), wanafunzi (1,917), walimu (193), walimu wakuu (5), viongozi wa dini (30), viongozi/mabingwa wa jamii (13), viongozi wa eneo husika (5), na vijana wa kujitolea (32). Aidha, wazazi wengine 2,607 (wanaume 1,115 na wanawake 1,492) walifikiwa kwa njia isiyo ya moja kwa moja, jambo linaloashiria kuenea kwa nguvu kwa ujumbe huo katika ngazi ya kaya nje ya kundi la awali.

Wakati huo huo, huko Bagamoyo, wazazi 1,464 walielimishwa, pamoja na angalau wanafunzi 40 wa Shule ya Msingi Nianjema, wanafunzi 54 wa mafunzo ya ufundi kutoka Chuo cha Biashara cha Baqwina, wanachama 92 wa vikundi vya kuweka akiba, na waumini 239 katika taasisi za dini; huku zaidi ya wanajamii 15,000 wakifikiwa pia kupitia matangazo ya Radio na Luninga na vyombo vingine vya habari.
Matokeo yanaonekanaje baada ya kampani? Baada ya Kampani hiyo kutekelezwa matokeo ya mabadiliko ya tabia yaliyoonekana kwa wazazi yalikuwa;- Mawasiliano bora ya familia; yaani wazazi sasa wanawashirikisha watoto katika mijadala ya ushirikiano kuhusu maamuzi ya masuala ya familia, pia kukuwa kwa mawasiliano baina ya wazazi na wanafamilia wengine, Kuonekana kwa mbinu chanya za nidhamu;yaani kuhama kutoka mbinu kali za nidhamu hadi mwongozo chanya kwa wazazi huunda nafasi kwa watoto kuuliza maswali na kushirikisha mawazo yao.
Sambamba na mabadiliko hayo mabadiliko mengine yaliyo onekana yalikuwa, wazazi kuanza kuhudhuria mikutano ya wazazi na walimu mara kwa mara shuleni, kufuatilia maendeleo ya kitaaluma, na kutafuta njia za kuboresha matokeo ya kujifunza kwa Watoto wao huku pia kukionekana kuimarika kwa wazazi kuwasaidia Watoto kujifunza nyumbani.
Aidha, ripoti hiyo pia inabainisha mabadiliko ya tabia za wanafunzi yaliyoonekana baada ya kampeni kutekelezwa ambayo ni;- Kukuwa kwa udadisi ulioimarika na mawazo makini miongoni mwa wanafunzi, yaani wanafunzi walionekana kukuza hisia kali ya uchunguzi na tabia ya kusoma na kuchambua vitabu kwa kujiamini shuleni na nyumbani, pia mahudhurio bora shuleni yaliyotokana na kupungua kwa utoro na kuchelewa, na kukua kwa uwezo wa kujieleza, Ubunifu na Kutatua Matatizo kwa baadhi ya wanafunzi.
Kwa mujibu wa Mtaalamu wa Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dr. Daniel Marandu, anasema kuwa Saikololojia inatuambia kwamba mtoto anapozaliwa na kuanza kukua anahitaji mbinu au maarifa yanayoweza kumsaidia mtoto kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Dr.Marandu anabainisha kwamba mbinu hizo, ndio hizi stadi za maisha. Anasema, watoto ambao wana kiwango kikubwa cha Stadi za Maisha wana nafasi kubwa sana ya kufanikiwa kimaisha ukilinganisha na wale ambao wana kiwango kidogo.
Naye Ofisa na Mtaalamu wa Mitaala kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania, Mwanahamisi Jokolo, alinukuliwa mwaka jana(2025) na wataalumu wa Uwezo Tanzania waliokuwa wakitengeneza video ya matokeo ya mradi wa Stadi za Maisha, alisema, ushirikiano kati ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Mashirika yasio ya kiserikali ni makubwa na mazuri ambayo kimsingi yatawezesha kuendelea kushirikiana kwa pamoja kusaidia kukuza stadi za maisha na maadili kwa wanafunzi huku akisisitiza kuwa stadi hizo ni muhimu sana kwa Watoto.
Kupitia mradi wa Stadi za Maisha na maadili, Uwezo Tanzania na Mashirika wadau wameweza kushikirikiana kikamilifu na serikali kupitia Wizara ya Elimu (Tanzania Bara na Zanzibar) Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na idara nyingine na kuhakikisha Stadi za Maisha zinachopekwa katika Mtaala ulioboreshwa, na pia walimu wanapatiwa mafunzo muhimu ya namna ya kuwasaidia watoto kukuza stadi hizo.
Ripoti ya utafiti wa Jumuiya ya vyuo vikuu vya Afrika Mashariki ya mwaka 2015, inaonesha, wahitimu wengi wa vyuo vikuu wana stadi za ujuzi mbalimbali lakini hawana stadi zinazowawezesha kutumia juzi hizo katika maeneo ya kazi. Tafiti hii inaonesha kwamba waajiri wengi walisema wahitimu wa chuo wanakosa stadi kama vile mawasiliano, ubunifu, kujitambua, utatuzi wa matatizo na fikra tunduizi hivyo walishindwa kuwaajiri katika nafasi mbalimbali. Wahitimu 6 kati ya kumi (sawa na asilimia 61 ya wahitimu wa chuo) hapa Tanzania walionekana kukosa stadi hizo muhimu na kupelekea kutopata ajira.
Kutokana na ripoti hizi inaonyesha umuhimu wa Mzazi na Mwalimu katika kujenga na kukuza stadi za maisha na maadili katika umri wa ukuaji na ngazi ya elimu-msingi, ambazo zitakuwa na faida kubwa kwa jamii.
Pia utafiti uliofanywa na Mradi wa Stadi za maiasha na Maadili (ALiVE) mwaka 2022, shule ilionekana kuchangia kwa asimilia kubwa ukuaji wa stadi za maisha. Vijana waliokuwepo katika madaraja ya juu ya elimu (sekondari) walionekana kuwa na umahiri wa juu zaidi wa stadi za maisha kuliko vijana waliokuwa katika madaraja ya chini (shule za msingi).
Tafiti hizi zimeweza kuchangia kuleta mabadiliko ya elimu na kufanya serikali kubadilisha mtaala na kuweka kipaumbele katika ukuzaji wa stadi za ujuzi na stadi za maisha katika mfumo wa elimu ili kuongeza uzalendo kwa vijana, kuwaongezea uwezo wa kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali kwa kutumia elimu wanayoipata na kubwa zaidi ikiwa kutatua tatizo la ajira katika nchi yetu.
Aidha, kutokana na umuhimu mkubwa wa stadi za maisha katika kujenga wananchi wazalendo, wenye uwezo wa kutengeneza ajira na wenye stadi za kuwawezesha kuendesha ajira mbalimbali, serikali imepitia mtaala wake na kufanya maboresho ya kuhakikisha kwamba stadi za maisha zimepewa kipaumbele katika mtaala ulioboreshwa.
Mtaala ulioboreshwa ambao umeanza kutumika kuanzia Januari 2024, umeweka kipaumbele katika stadi tano za maisha ambazo zimechopekwa katika masomo mbalimbali ili kuweza kuzikuza. Stadi hizo ni pamoja na fikra tunduizi, utatuzi wa matatizo, mawasiliano na Ushirikiano.
Kwa maboresho haya, elimu itamjenga mwanafunzi mwenye uwezo wa kutumia yale anayojifunza katika masomo katika kukabiliana na hali mbalimbali za maisha kama vile: kuwa na mahusiano bora na wengine katika jamii, kukabiliana na changamoto kama vile ukosaji wa ajira, kuweza kushirikiana na watu kutoka jamii mbalimbali ili kuweza kufanya maendeleo ya ukuzaji uchumi na kuleta amani katika jamii wanazoishi kwa ujumla.
Maswali ya kujiuliza ni; Je wewe kama mzazi unafanya nini ili kumsaidia mtoto wako ili kukuza stadi hizi muhimu za maisha ? Umejifunza nini kutoka katika Makala haya? Tupe maoni yako kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno kupitia anuani ya jarida hili.

Be the first to comment