Baada ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutangaza marekebisho ya ratiba ya upimaji na mitihani ya Taifa kwa mwaka 2026, kwa lengo la kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na uwezekano wa mvua kubwa za El Nino zinazotarajiwa katika baadhi ya maeneo nchini, wadau wa elimu nchini Tanzania wameipongeza serikali kwa uamuzi huo huku wakisema kuwa ni hatua sahihi kwa sababu ni vizuri kuchukua tahadhari mapema.
Baadhi ya wadau waliozungumza na jarida hili, wamesema mabadiliko haya ni sahihi huku wakisisitiza kwamba usalama na ustawi wa wanafunzi, walimu na jamii kwa ujumla unapaswa kuwa kipaumbele.
Akizungumza na mwandishi wa jarida hili, Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi Martha Makala alisema kuwa kubadilishwa kwa ratiba ya mitihani ni uamuzi mzuri kwa ajili ya ulinzi na usalama wa mtoto, huku akiongeza kuwa elimu inaendelea hata baada ya mtoto kuhitimu hatua fulani ya masomo.
Naye, Evena Massae, Mkurugenzi wa shirika lisiso la kiserikali-COSUPED, lililopo Dar es Salaam Tanzania, ameliambia jarida hili kuwa, kubadilishwa kwa ratiba za mitihani ni hatua sahihi kwa sababu ni vizuri kuchukua tahadhari ukizingatia na baadhi ya miundombinu ya shule kwenye baadhi ya maeneo hasa vijijini, kuliko kuhatarisha maisha ya wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine.
Pia amesema, kiuhalisia barabara nyingi hasa za vijijini hazina ubora kwa hiyo zinaweza kuharibika na kutopitika wakati wa mvua nyingi.
Aidha, ameongeza kuwa, kutokana na hali hiyo maandalizi ya wanafunzi kwa mitihani itakayofanyika yapewe kipaumbele ili ifanyike kikamilifu na kwa ufanisi, pia wanafunzi wapewe muda wa kutosha wa kujiandaa na mitihani.
Sambamba na hayo, Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Shirika lisilo la kiserikali(NGO) la Transforming Life (TL),Bi, Nashivai Mollel, akizungumza na mwandishi wa jarida hili amesema kwa mtazamo wake kama mdau wa elimu, amepokea mabadiliko haya kwa kuelewa kwamba usalama na ustawi wa wanafunzi, walimu na jamii kwa ujumla unapaswa kuwa kipaumbele, hivyo mvua za El Niño zinaweza kuleta changamoto katika usafiri, mahudhurio au kuathiri mazingira salama ya kufanyia mitihani, ni muhimu mamlaka kuchukua hatua za tahadhari mapema.
Amesema, ni muhimu pia kuhakikisha kuwa mabadiliko haya hayawaongezei wanafunzi msongo wa mawazo au kuvuruga maandalizi yao.
“Kwa wanafunzi waliopo katika madarasa ya mitihani, ushauri wangu ni kuendelea kutumia muda huu kwa maandalizi vizuri, kupitia mada muhimu, kufanya mazoezi ya mitihani iliyopita na kuwasiliana na walimu pale wanapohitaji msaada. Walimu nao waendelee kuwa karibu na wanafunzi, kutoa mwongozo wa kitaaluma na kihisia, na kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata taarifa sahihi kuhusu ratiba na maandalizi ya mitihani.” Amesema Bi, Nashivai Mollel.
Aidha amesisitiza kuwa, usalama wa wanafunzi, walimu na jamii ni kipaumbele cha Kwanza hivyo anakubaliana kabisa na kuunga mkono uamuzi huo wa serikali.
Pia, Bw. Nicodemas Etlawe, Mkurugenzi Mkuu, Maarifa ni Ufunguo NGO, Arusha ameliambia jarida hili kuwa kubadilishwa kwa ratiba ya mitihani ni uamuzi mzuri kwa sababu ya nia ya kuepusha madhara makubwa kwa wanafunzi na walimu.
“Hata hivyo, kuna mambo ya kuzingatia kama Je, walimu wamemaliza kufundisha mitaala yote? Je, NECTA wamepewa muda wa kutosha kutunga mitihani? .” Alisema, Bw. Etlawe.
Tangazo la marekebisho ya ratiba ya upimaji na mitihani ya Taifa kwa mwaka 2026, lilitangazwa jijini Dar es Salaam, Septemba 25, 2026, na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, huku akisisitiza kuwa hatua hiyo imechukuliwa baada ya Serikali kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa na kutathmini athari zinazoweza kujitokeza katika uendeshaji wa upimaji na mitihani ya Taifa.
Alisema kwa mujibu wa utabiri rasmi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, kuna uwezekano wa kutokea kwa El Nino yenye nguvu, huku mvua zikitarajiwa kuanza katika baadhi ya maeneo mwezi Oktoba 2026 na kuwa nyingi zaidi mwezi Novemba 2026, hali ambayo inaweza kuathiri usafiri na kufikika kwa baadhi ya vituo vya mitihani.
Ameeleza kuwa kwa kuzingatia jiografia ya nchi na uwezekano wa baadhi ya maeneo kukumbwa na mafuriko, changamoto za usafiri na athari nyingine zinazoweza kusababishwa na hali ya hewa, Wizara kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani la Tanzania imefanya marekebisho ya ratiba ya upimaji na mitihani ya Taifa.
Kwa mujibu wa ratiba iliyorekebishwa, Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili Ngazi ya Shule utafanyika Oktoba 7 hadi 8, 2026, wakati Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne utafanyika Oktoba 5 hadi 6, 2026.
Aidha, Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili utafanyika Oktoba 12 hadi 23, 2026, huku Mitihani ya Kidato cha Nne ikifanyika kuanzia Oktoba 19 hadi Novemba 6, 2026.
Amesema marekebisho hayo yanalenga kuhakikisha usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi, maafisa na wadau wengine wanaohusika na uendeshaji wa mitihani, pamoja na kulinda mitihani, vifaa na nyaraka muhimu.

Be the first to comment